Anaondoka Okwi kinakuja Chuma





SIMBA inajiandaa na mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe lakini hawakajakaa kimya kwenye mpango mzima wa usajili kwa ajili ya msimu ujao ambapo wanahitaji kuiboresha zaidi timu yao.

Wakati baadhi ya wachezaji wanatajwa kutua Simba msimu ujao wa Ligi Kuu lakini kuna baadhi ya wachezaji ndani ya mabingwa hao watetezi wa ligi wataondoka baada ya kupata madili mengine huku wengine huenda wakaachwa. Mmoja wa nyota ambaye huenda ataondoka msimu ujao ni Mganda Emmanuel Okwi ambaye anatajwa kuwaniwa na Super Sport inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini.


Okwi alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda baada ya kuvunja mkataba wake na SønderjyskE ya Dernmak na sasa mkataba wake Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu huku ikitajwa dili lake hilo linakwenda vizuri. Mwaka jana, timu ya Kaizer Chief ya Afrika Kusini nayo ilituma maombi Simba ya kutaka kumnunua mshambuliaji huyo lakini waligonga mwamba baada ya uongozi wa Simba kutaja dau kubwa. Simba walihitaji Dola 150,000 (zaidi ya Sh 300 milioni).

Habari ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka ndani ya Simba ni kwamba Okwi ambaye ni kipenzi cha Wanasimba ni kama amewagawa mabosi wake ambapo baadhi wanataka aongezewe mkataba mpya huku wengine wakiruhusu mchezaji huyo kuondoka mkataba wake utakapomalizika.

Okwi ana ofa nyingi mezani lakini imeelezwa kwamba ofa ambayo anaipa kipaumbele baada ya uongozi wa Simba kumchunia ni SuperSport. Wakati Okwi anatajwa kupata dili jipya Sauzi, huku nyuma Simba inataka kufanya mazungumzo ya awali na Ibrahim Ajibu wa Yanga, Obrey Chirwa wa Azam FC, Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia ya Kenya pamoja na Lazarous Kambole wa Zesco United ya Zambia. Wakiwapata hao basi pengo la Okwi kama ataondoka kweli huenda likazibwa.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema masuala ya usajili yote yatakuwa chini ya kocha wao, Patrick Aussems ambaye ndiye atakayetoa orodha ya wachezaji wa kuwasajili kulingana na mapungufu katika sehemu mbalimbali ndani ya timu yao.

Rweyemamu alisema: “Kocha ndiye mwenye jukumu la kusajili kulingana na mahitaji ya timu, atapendekeza wachezaji wapya anaowahitaji na kwa nafasi anazotaka ziboreshwe, lakini kuna wale ambao mikataba yao itakuwa imemalizika au wanatamani kwenda kutafuta changamoto timu nyingine nao tutawapa ruhusa.

“Simba sasa hivi imefikia mbali na imepiga hatua ndiyo maana tumecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na usajili ambao tutaufanya utakuwa wa siri tena kwa sura ambazo hazifahamiki hapa nchini kwa wachezaji wanaocheza hapa ndani au wa kigeni,”

alisema Mwenyekiti wa Simba, Swed Mkwabi alisema Bodi ya Wakurugenzi inafahamu kuna wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao mikataba yao inamalizika lakini hakuna mchezaji waliyezungumza naye kuhusu mkataba mpya na watafanya hivyo pale ambapo mikataba yao itafika kikomo. Mkwabi alisema hakuna mchezaji yeyote ambaye wamepokea ofa kutoka timu nyingine kwa maana hiyo hakuna mchezaji aliyepewa ruhusa ya kuondoka na kusaini timu nyingine kwani wao wamejipanga kuwapa mikataba mipya hapo baadaye. “Okwi ni miongoni mwa wachezaji ambao mikataba inamalizika, hilo lipo ndani ya uwezo wetu na tutalifanyia kazi,” alisema Mkwabi.





LWANDAMINA ASHITUKA

Wakati vuguvugu la usajili likiendelea ndani ya Simba na timu nyingine, mshambuliaji Kambole wa Zesco United ya Zambia naye ameweka wazi mipango yake ya kutua Simba huku kocha wake George Lwandamina akisema endapo mabingwa hao watetezi wa ligi nchini watamchukuwa mchezaji wake litakuwa ni pigo kubwa kwenye klabu yake.

Lwandamina ambaye aliwahi kuifundisha Yanga, ameshtushwa na taarifa za usajili huo baada ya kuwa miongoni mwa watu wanaovutiwa na uwezo wa Kambole. Lwandamina aliliambia Mwanaspoti kuwa taarifa za mchezaji wake kuhitajika Simba zinampa wakati mgumu wa kuanza kusaka mbadala wake kwani ni mchezaji ambaye ana mchango mkubwa kwenye kikosi chake.

“Mbona sijui, ni mchezaji mzuri sana na amekuwa na mchango mkubwa katika timu yangu, bado nahitaji kumuona akiendelea kuwa katika kikosi changu,” alisema. Aliongeza kama kweli mchezaji huyo ataondoka itakuwa ni hatua nzuri katika maisha yake ya mpira. Kwa upande mwingine, kiungo Clatous Chama aliyewahi kucheza pamoja na Kambole akiwa Zesco United kabla ya kutua Simba, alisema kama wakifanikiwa kumsajili nyota huyo litakuwa ni jambo zuri kwao. “Lazaorus ni mchezaji mzuri na timu yoyote itakayompata itafurahia huduma yake, ana nidhamu lakini pia ni mpambanaji kwa muda wote anapokuwa uwanjani,” alisema.

Naye mshambuliaji Juma Liuzio aliyewahi kuchezea Zesco United na Simba, aliliambia Mwanaspoti kama Simba ikimpata mchezaji huyo kipindi hiki itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa. “Yule jamaa ana kasi sana na hivi sasa yupo katika kiwango kizuri, kama kweli ikimsajili basi itakuwa imepata mtu sahihi na atawasiadia,” alisema Liuzio.

KAMBOLE AFUNGUKA

Mwanaspoti lilimtafuta Kambole ili kujua ukweli kuhusu ya usajili wake ndani ya Simba, alisisitiza: “Hakuna mawasiliano ya hivyo yaliyofanyika mimi na wao, sijawaona labda kama wameenda moja kwa moja katika klabu, kwangu hawajafika.” Aliongeza bado hatma yake kama ataendelea kubaki Zesco United au atajiunga na Simba kwani bado ana mkataba na timu yake ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu na ndipo atafanya uamuzi.1

Post a Comment

0 Comments