Aussems : Sijawahi kutolewa robo Fainali
KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema kuwa katika historia yake ya kufundisha soka, hajawahi kushindwa baada ya kutinga robo fainali.
Aussems, ameyasema hayo alipozungumza nasi jana, ikiwa ni siku chache kabla ya kikosi chake kuivaa TP Mazembe katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa jijini Lubumbashi, DR Congo, Jumamosi.
“Katika historia yangu ya soka na timu ambazo nimewahi kufundisha, nilizivusha hatua ya robo fainali, ndio maana sina hofu na hili kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa,” alisema Aussems.
Aussems alisema anatambua ni makosa madogo waliyoyafanya katika mchezo wa kwanza na kwamba amejipanga kikamilifu kukabiliana na mchezo huo.
“Natambua kuwa Watanzania na mashabiki wa Simba walikuwa na hofu pengine tungefungwa mabao mengi na TP Mazembe katika mchezo uliopita, lakini wameshuhudia namna tulivyopambana, sidhani kama tunaweza kushindwa mchezo wa marudiano.
“Pengine hofu kubwa ni kwa sababu tutakuwa ugenini, mimi naamini kuwa mpira ni dakika 90, hata tuwe wapi ni plani yangu na juhudi za wachezaji ndizo zitakazoleta matokeo mazuri,” alisema Aussems.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita, timu hizo zilitoka suluhu hivyo ili Simba iweze kusonga mbele, inahitaji ushindi au sare ya mabao.
0 Comments