NA SALEH ALLY
KWANZA lazima tukubali Simba walikuwa na kila sababu ya kuhoji kuhusiana na uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kuamua kuadili mwamuzi.
Caf wamembadili mwamuzi Bamlak Tessema Weyesa kutoka Ethiopia bila ya kutoa sababu za kutosha na badala yake nafasi yake imechukuliwa na mwamuzi Janny Sikazwe wa nchini Zambia.
Mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Robo Fainali kati ya TP Mazembe dhidi ya Simba inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka katika nchi hizi mbili, yaani Tanzania na DR Congo.
Pamoja na hivyo, mechi hiyo inaendelea kuwa maarufu sana kwa kuwa inaikutanisha timu ambayo inaonekana kupata sifa ya “Kiboko cha Vigogo” hasa inapocheza nyumbani kwao dhidi ya mmoja wa vigogo wa Afrika.
Simba inaonekana inapokuwa nyumbani kwake Dar es Salaam, hakuna nafasi kwa timu yoyote hata kama ni kubwa vipi, na imeweza kudhihirisha hilo huku ikiibuka na ushindi dhidi ya vigogo kama Al Ahly, AS Vita na Mazembe wamekuwa timu pekee ambao hawakupoteza mchezo.
Wakati Mazembe walitua Dar es Salaam wakiwa wanajiamini sana, hakuna ubishi kwamba wameondoka na hofu kutokana na walichokiona kutoka kwa Simba ambao pamoja na sare ya bila kufungana, uchezaji wao ulionyesha ni timu hasa ambayo inaweza kupambana.
Sasa mwamuzi kutoka Ethiopia kama alionekana ni wa Afrika Mashariki na anaweza kuwa na undugu na Simba, vipi mwamuzi kutoka Zambia ambayo ni pua na mdomo na Lubumbashi? Yote ni ya kujiuliza lakini halipaswi kuwa na nafasi kubwa sana utafikiri hayo ndio maandalizi.
Simba wana kila sababu ya kuzungumza na tayari wameshafanya hivyo, inaweza ikawa ni sehemu ya tahadhari lakini viongozi hawapaswi kuendelea kulizungumza hilo hadi kufikia hali ya kujiondoa relini.
Nasema hivyo nikiwasisitiza kuwa makini kwa kuwa kama wataendelea hivyo, mwisho hili linaweza kuingia kwenye vichwa vya wachezaji wanoaweza kuanza kuamini kama wamekuwa wanaonewa na mwisho wakawa na mechi mbaya.
Wachezaji wanaweza wakawa wamelisikia hilo na wanachotakiwa ni kuwaachia wahusika washughulike na suala hilo halafu wao wakaendelea na kazi yao ya kucheza mpira na kutafuta ushindi kwa sababu ya kikosi chao.
Uamuzi wa kubadili refa hauwezi kuwa jibu la Simba katika kipindi kilichobaki, wamesema wamesikika na ilikuwa sahihi kusema lakini sasa wanapaswa kutupa nguvu nyingi katika maandalizi yao ya mwisho kabla ya kuivaa Mazembe, kesho ikiwa nyumbani kwake.
Mazembe lazima watakuwa wanaendelea kujiandaa na tena itakuwa kwa nguvu kwa kuwa hawawezi kusema watakaa wanaisubiri Simba wakitegemea mchekea. Tayari wameishaona kazi si rahisi, hivyo watajipanga hasa kuhakikisha wanashinda.
Kama TP Mazembe watakuwa wanajipanga vilivyo, vipi Simba waone suala la refa ni kubwa sana? Huenda lilifanyika makusudi kuwavuruga maana walijua pale atakapotangazwa mwamuzi lazima Simba wataekeleza nguvu kwenye kulalamika.
Hata kidogo Simba hawapaswi kuingia katika mtego huo na badala yake wapambane kuyafanyia kazi matatizo ambayo yanawafanya waonekane kama wanayumba. Waanzie katika safu ya ulinzi kuhakikisha wanacheza vizuri na kubadili mambo.
Simba wamekuwa hawajiwezi katika ulinzi wanapotoka nje ya nyumbani. Angalia ndani ya mechi tatu wamefungwa mabao 12 ya ugenini. Kama watashindwa kuibadili hii, basi watakang’olewa bila hata ya ubishi.
Wakikomaa na hilo, basi wanaweza zaidi kuleta mapinduzi kwa kufanya kile ambacho hakikuwa kimetarajiwa na wengi.
Wachezaji waendelee kujikita katika kile kinachoaminika ndiyo kinahitajika kufanyika ili kuisaidia Simba kuing’oa Mazembe badala ya wao kutumika kama sehemu ya kujiangamiza.
from sokoa news http://bit.ly/2VFtx3D
1


0 Comments