Kocha Yanga afunguka sare ya Ndanda FC





Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema mambo mawili ikiwemo kukosa umakini yamechangia kushindwa kupata pointi tatu dhidi ya Ndanda FC.


Yanga jana ililazimisha sare ya bao 1-1 na Ndanda, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.


Akizungumza muda mfupi baada ya mpira kumalizika, Zahera alisema wachezaji walikosa umakini hasa kipindi cha kwanza.


Alisema watajilaumu wenyewe kwa kuziacha pointi mbili ugenini ambazo walikuwa na uwezo wa kuzipata endapo wachezaji wake wangecheza kwa nidhamu.


Pia alisema uwanja huo haukuwa rafiki kwa wachezaji kucheza kwa umakini ingawa alikwepa kutoa lawama kwa mwamuzi wa mchezo huo.


“Hakuna mtu wa kumlaumu. Sisi wenyewe tunapaswa kujilaumu, tumeshindwa kupata pointi tatu kwa sababu ya kukosa umakini.


“Lakini uwanja nao haikuwa mzuri, wachezaji walipata taabu kumiliki mpira. Kuhusu mwamuzi siwezi kutoa lawama kwake mimi naona alichezesha vizuri, penalti ya kwanza ilikuwa sahihi ile ya pili mtaangalia marudio kama ilikuwa ndani ya boksi au nje,” alisema Zahera.


Katika mchezo huo, safu ya ulinzi ya Yanga ilikosa nidhamu ya mchezo hasa mabeki wa kati Kelvin Yondani na Andrew Vincent ‘Dante’ ambao mara kwa mara ‘walipotea’ uwanjani.


Yondani alifanya kosa la kushindwa kumiliki mpira uliokuwa katika himaya yake kabla ya kuzidiwa maarifa na Vitalis Mayanga aliyefunga dakika ya 19.


Mayanga aliyekuwa akimsumbua Yondani na Dante, alifunga bao hilo baada ya kumpiga chenga kipa Klausi Kindoki kabla ya kutumbukiza mpira wavuni.


Kipindi cha kwanza Yanga ilionyesha udhaifu katika idara ya ulinzi na ushambuliaji iliyoshindwa kufunga mabao licha ya Ndanda kucheza mchezo wa kujilinda muda mrefu.


Kipindi cha pili Yanga ilichangamka baada ya Zahera kumtoa Amissi Tambwe aliyekosa penalti dakika ya 29 na nafasi yake kujazwa na Deus Kaseke.


Penalti hiyo ilitokana na Heritier Makambo kufanyiwa madhambi na Baraka Majogoro ndani ya 18. Mchezaji wa kiungo Papy Tshishimbi aliifungia bao Yanga kwa kichwa dakika ya 61 akiunganisha mpira wa krosi uliopigwa kutoka upande wa kushoto na Yondani.


Yanga imefikisha pointi 68 ikiizidi Simba pointi 11 lakini Wekundu hao wa Msimbazi wana mechi saba mkononi.


Yanga imeendelea kupata wakati mgumu inapocheza dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wa huo kwani mara nne ambazo timu hizo zimekutana ukiwemo mchezo wa jana, Yanga imeshinda mara moja msimu uliopita iliposhinda mabao 2-1.


Sare hiyo inaendeleza rekodi bora ya Ndanda inapocheza uwanja wa nyumbani kwani katika michezo mitano ya hivi karibuni imeshinda yote.


Ndanda iliifunga KMC mabao 2-0, iliichapa Singida United 2-0, iliinyuka Alliance bao 1-0, iliifunga Kagera Sugar 2-0 kabla ya kuilaza JKT Tanzania 2-1.


Mara ya mwisho Ndanda kupoteza mchezo kwenye uwanja huo ilikuwa Januari 7, mwaka huu ilipokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.


Yanga ilikuwa ikipata taabu kupata ushindi kwenye uwanja huo hadi ilipovunja mwiko Februari 28 mwaka jana iliposhinda mabao 2-1.
1

Post a Comment

0 Comments