Yanga hii ni “Iyena iyena” yaibamiza Kagera Sugar,Makambo aendelea kumwacha mbali Kagere.

.Ni mwendo Vichapo tu,baada ya timu ya Yanga kuendeleza ubabe dhidi ya Kagera Sugar kwa kupata ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Haritier Makambo alifunga bao moja katika mchezo huo na kufikisha mabao 15 hivyo kumpita mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere mwenye mabao 14 huku akibakiza bao moja kumfikia kinara wa ufungaji Salum Aiyee wa Mwadui FC  mwenye mabao 16.

Jambo lililovutia katika mchezo wa jana ni baada ya  Makambo  raia wa Congo kufunga bao kisha kumfuata beki Kelvin Yondani na kupiga goti mbele yake na kuanza kumfuta kiatu kwa jezi yake.

Yondani ndiye aliyempa pasi ya bao Makambo  akipiga mpira mrefu kutoka nyuma na kumkuta Mcongo huyo aliyemalizia kwa kichwa.

Pia Yondani  ndiye aliyempa pasi ya bao la kwanza kwanza Makambo katika mchezo uliopita dhidi ya AFfrican Lyon ambayo Yanga ilishinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Mcongo huyo.

Pasi hiyo ya Yondani katika mchezo uliopita imefanana vile vile na pasi aliyotoa kwa Makambo katika mchezo wa jana.

Hata hivyo Yondani alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 82 na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro baada ya kumpiga kiwiko Kassim Hamis wa Kagera Sugar.

Mechi ilivyokuwa.

Yanga ambayo imefikisha pointi 74 ilianza mchezo huo taratibu na dakika ya tisa tu  ilijikuta ikipata kashikashi golini kwake baada ya Kagera Sugar kupata  kona iliyopigwa na  David Luhende na kuokolewa na mabeki .

Timu hiyo ilijibu mashambulzii dakika ya 22 baada ya Heritier Makambo kuachia shuti kali lililodakwa na kipa Jeremia Kisubi.

Paul Ngalyoma aliipatia Kagera Sugar bao kwa kichwa dakika ya 30 akimalizia mpira wa kona uluiopigwa na Ally Ramadhani.

Yanga ilijibu mapigo dakika ya 33 baada ya kona iliyopigwa na Thaban Kamusoko kutua kichwani mwa  Papy Tshishimbi na mpira huo  kumchanganya mchezaji wa Kagera Sugar,Kassim Hamis ambaye alijifunga wakati anajitahidi kuokoa.

Dakika ya 47 Makambo aliwanyanyua vitini mashabiki wa  Yanga baada ya kufunga bao la kichwa akimaliza pasi ya mbali ya Yondani.

Kassim Hamis alisahihisha makosa  ya kujifunga baada ya dakika ya 57 kuisawazishia timu yake Kagera Sugar bao la pili kwa shuti kali ndani ya 18 lililomshinda kipa Klaus Kindoki ambaye aliruka na kuugusa kidogo mpira huo lakini akajikuta akiusukumizia nyavuni.

Yanga iliendelea kupambana na kufanikiwa kuandika bao la tatu lililofungwa na Thaban Kamusoko dakika ya,74  kwa faulo ya moja kwa moja iliyokwenda  nyavuni.

Huo unakuwa mwendelezo wa Kagera Sugar kuendelea kuwa wateja wa Yanga katika michezo ya karibuni.

Katika mechi tano ambazo timu hizo zimekutana tangu  2016,Yanga imeonekana mbabe wa Kagera Sugar kwani ilishinda mechi zote.

Oktoba 20,2016 Yanga ilishinda mabao 6-2 ugenini,Mei 9 mwaka 2017 iliichapa Kagera Sugar mabao 2-1,Oktoba 14,2017 Kagera ililala kwa mabao 2-1,Machi 9,2018 Yanga ilihishinda mabao 3-0 na mechi ya mzunguko wa kwanza msimu huu Yanga ilishinda kwa mabao 2-1




from sokoa news http://bit.ly/2G9dBQx
1

Post a Comment

0 Comments