
DIRISHA kubwa la usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, limeanza kunukia baada ya baadhi ya klabu kuingia katika mawindo ya kusaka nyota wa kuwasajili.
Licha ya kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halijatangaza rasmi kuanza kwa msimu mpya wa usajili, tayari baadhi ya klabu zimeanza usajili wa awali kwa lengo la kuboresha vikosi vyao.
Usajili mpya wa wachezaji unatarajia kuanza rasmi baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, ambapo timu zote 20 zitashuka uwanjani kesho kufunga pazia la ligi hiyo.
Kuanzia hapo, klabu zitahamia katika vurugu za usajili ambazo tayari zimeanza kusikika hasa kwa klabu kubwa zenye ushindani wa soka nchini, Simba na Yanga.
Huku kukiwa na tetesi za Yanga kuwanasa nyota mbalimbali; wazawa na kigeni, usajili kamili unatarajiwa kuanikwa keshokutwa wakati Ligi Kuu Bara ikiwa imemalizika.
Katika kikosi kipya cha Yanga, tunatarajia kuona sura mpya baada ya baadhi ya wachezaji kutokuwa na uhakika wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Nafasi kama ya ushambuliaji, viungo na mabeki itaongezwa wachezaji wengine ili kuboresha timu ambayo kwa misimu miwili haijafanya vizuri.
Yanga wakionekana kudhamiria kufanya mabadiliko ndani ya kikosi chao, lakini wapinzani wao Simba nao wapo katika mawindo makali ya kusajili nyota ambao wataitangaza nchi katika anga za kimataifa.
Kwa kuwa kipindi kinachokuja ni cha mavuno kwa wachezaji walio wengi hasa kwa wale walioonyesha viwango katika msimu unaomalizika, lakini wanatakiwa kuwa makini na mikataba ya awali wanayokubaliana na klabu zinazowahitaji.
Tumeshuhudia unapofika msimu wa usajili, wachezaji wengi wanakurupuka kusaini mikataba pasipo kujua haki zao na mwisho wa siku wanajikuta wameingia katika matatizo ya kutolipwa.
Mifano ni mengi kwa wachezaji ambao walikurupuka kusaini mikataba kwa kipindi kama hicho kinachokuja na mwisho wa siku kuwa ni usumbufu mkubwa wa kupata stahiki zao.
Msimu unaomalizika kulikuwa na kesi nyingi za wachezaji kudai fedha zao za usajili kutoka kwa klabu mbalimbali za Ligi Kuu Bara, ili tatizo hilo lisijitokeze ni vizuri wakawa makini katika kusajili mikataba.
from sokoa news http://bit.ly/2QwWXiQ
1

0 Comments