HUKO Jangwani mashabiki wanachekea tumboni baada ya jana kuwashuhudia watani zao, Simba wakibanwa mbavu na Azam na kuwarahisisha kazi na kurejea tena kileleni mwa Ligi Kuu Bara kama jioni ya leo Jumanne itapata ushindi mbele ya Ruvu ShootingSimba ililazimishwa suluhu na Azam kwenye Uwanja wa Uhuru na kuifanya ipoteze alama tano katika mechi zake mbili zilizopota, ikianza kwa kichapo dhidi ya Kagera Sugar na kuzidi kuwapa tumaini Yanga kuwapoka ubingwa wanaoshikilia kwa sasa.
Vinara hao wamefikisha alama 82 baada ya mechi 33 na kama Yanga leo itashinda ina maana itarejea kileleni kwa kufikisha pointi 83 kutokana na mechi 36 na hivyo, kuzidi kuufanya ubingwa wa ligi kutokuwa na mwenyewe.
Mashabiki wa Simba walijikuta wakiishiwa pozi baada ya kushuhudia timu yao ikibanwa na Azam ambao, wanashika nafasi ya tatu na alama zao 69 baada ya mechi 36 na waliofungwa mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa na malengo tofauti kwa timu zote mbili ambapo Simba kama ilivyo, waliingia na hesabu za kusaka ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Lakini, kwa Azam, pamoja na kutokuwepo kwenye mbio za ubingwa, mchezo wa jana ulikuwa ni kujiimarisha nafasi ya tatu, kulinda heshima pia kumaliza unyonge mbele ya Simba ambao, hawajawafunga katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu walizokutana kwa miaka miwili na miezi mitatu.
Ingawa walikuwa na malengo tofauti, lakini timu hizo ziliingia uwanjani zikionekana kuwa na tamaa ya kusaka ushindi na hata namna mpangilio wa vikosi vyao, ulionyesha wazi kuwa mpango kabambe ni kushambulia na sio kujilinda.
Timu zote zilianza na mfumo wa 4-4-2 huku vikosi vyao vikiwa na kundi kubwa la wachezaji ambao, aina ya soka lao ni kushambulia Azam wakiwa na mawinga asili wawili na washambuliaji wawili pamoja na kiungo mmoja mshambuliaji.
Upande wa Simba, walianza na viungo wanne lakini kati yao watatu ni wa ushambuliaji ikionekana ni mkakati wa kuhakikisha wanamiliki zaidi mpira na kutengeneza nafasi.
Upangaji huo wa vikosi ulishabihiana na kile kilichotokea ndani ya uwanja kwani, timu hizo zilicheza soka la kushambuliana kuanzia dakika ya mwanzo ya mchezo ingawa mara kwa mara hali ya uwanja ilikuwa na maji kwenye baadhi ya maeneo ilitibua mipango ya timu hizo kusaka mabao.
Hata hivyo, licha ya kumiliki mpira na kushambuliana kwa zamu, washambuliaji wa pande zote mbili walionekana kukosa utulivu na kupoteza nafasi kadhaa ambazo wangeweza kuzitumia kupata mabao.
Miongoni mwa nafasi nzuri ambazo Azam walizipata kipindi cha kwanza ni ile ya Donald Ngoma aliipoteza dakika ya 29, ambapo akiwa analitazama lango, alipiga shuti lililopaa baada ya kupokea pasi nzuri ya chinichini kutoka kwa Bruce Kangwa.
Shambulizi la Ngoma lilikuwa kama ni kulipa lile lililofanywa na Simba dakika mbili kabla kupitia Meddie Kagere, ambaye alipiga shuti lililodakwa na kipa wa Azam, Razak Abalora, baada ya kupokea pasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Katika kipindi hicho cha kwanza, refa Hance Mabena kutoka Tanga, aliwaonyesha kadi za njano wachezaji Joseph Mahundi na Obrey Chirwa wa Azam FC kwa kuwachezea faulo wachezaji wa Simba.
Katika hali ya kushangaza, dakika ya 34 ya mchezo, Aggrey Morris alimpiga kiwiko Kagere lakini tukio hilo halikuonwa na waamuzi ingawa Simba walionekana kulilalamikia.
from sokoa news http://bit.ly/2LHFkOB
1

0 Comments