Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amewataka wabunge na madiwani wa viti maalumu kusimamia rasilimali za umma ili zinufaishe wananchi wote.
Akizungumza Jijini Mwanza katika semina ya kujenga uwezo kwa viongozi wanawake wa serikali za Mitaa (WASEMI) iliyoandaliwa na shirika la TGNP Mtandao, Makinda alisema mchango wa wabunge na madiwani wa viti maalumu umekuwa hauonekani vizuri au kutambuliwa na jamii kutokana na wao kutokujiamini kitu ambacho kimechangia kuwarudisha nyuma na kushindwa kuendelea mbele.
"Tatizo sisi viongozi wanawake, tunajenga hofu, tunaogopa kujitokeza na kuwajibika vizuri kwa wananchi kwa sababu ni viti maalum. Sisi tulianzia pia viti maalumu, lakini tulipata nafasi ya kwenda jimboni kwa sababu tulijiamini, tuliwajibika kikamilifu na tulihakikisha uwezo wetu unaonekana na kila mtu. Jitokeze kwa wananchi, watumikie kwa uadilifu, watakuona na kutambua mchango wako,"alisema.
Aliwaasa wanawake viongozi wa serikali za mitaa, kusimamia ubora wa huduma za jamii katika halmashauri zao na kuhakikisha kinachofanyika huko wanakielewa vizuri na kutoa taarifa kwa wananchi.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Viongozi wa serikali za Mitaa (WASEMI) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Kibena Kingo amesema watahakikisha wenyeviti wa halmashauri wanawake wanaonesha mfano bora wa utendaji uliotukuka kwenye halmashauri zao kwa kutokomeza rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na kuhakikisha kila senti iinaboresha maisha ya jamii.
"Ndugu zangu, viongozi wanawake wa halmashauri na madiwani, sisi wanawake tumeaminiwa tukapewa nafasi, tusimamie vizuri rasilimali za halmashauri zetu, tujenge mtandao kutokomeza ukatili wa kijinsia, tutenge bajeti nzuri inayozingatia usawa wa kijinsia na kuboresha maisha ya wote bila ubaguzi,"alisema.
Mkutano huo ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa TGNP Mtandao na WASEMI ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Serikali za Mitaa ALAT, Gulamhafeez Mukadam na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Anjelina Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza.
from sokoa news https://ift.tt/32Ud1Rz
1
0 Comments