Mabasi mawili yakiwa na abiria zaidi ya 85 yakamatwa


Katika muendelezo wa  operesheni ya ukaguzi wa Mabasi na Malori Mkoani Arusha iliyoanza tarehe 09.07.2019, leo tarehe 18.07.2019 muda wa mchana huko katika maeneo Kona ya Engaruka – Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli  Katika barabara inayoelekea Loliondo mabasi mawili moja la Kampuni ya Coastal Line  na lingine la Kampuni ya Loliondo  yalikamatwa yakiwa yamezidisha Abiria zaidi ya 85.

Akiongea na Waandishi wa Habari Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP)Joseph Bukombe amesema basi la kampuni ya Coastal Line lenye namba za usajili T. 447 ADR lilikamatwa likiwa  na abiria 87, ambapo abiria 22 walikua wamezidi katika basi hilo badala ya 65 ambao ndio uwezo wa gari. Basi la Kampuni ya Loliondo lenye namba za usajili T.
919 BRA lilikamatwa likiwa na abiria 66 badala ya abiria 60 ambapo abiria 6 walikuwa wamezidi.

Amesema saivi madereva na makondakta  wa mabasi wamebuni mbinu  nyingine ambapo wakati wa ukaguzi kabla ya kutoka stendi ya mabasi wanakua wamebeba levo siti, lakini wakiwa njiani hasa wakishavuka vituo vya ukaguzi wanaamua kubeba abiria wengi zaidi.

Aliendelea kusema saivi wameamua kufanya operesheni hiyo katika maeneo mbalimbali bila ya ubaguzi nje kabisa ya mji kwa lengo hasa la kuwakamata wote wanaokiuka sheria na taratibu zilizowekwa hasa wenye  tabia ya kubeba abiria zaidi na kuendesha magari yakiwa mabovu.

“Leo tumeamua kufanya ukaguzi nje kabisa ya mji, ka mnavyoona tupo huku maeneo ya Mto wa Mbu na tumeyakuta mabasi haya yakiwa yamezidisha abiria.Tunaendelea kuwataka wamiliki pamoja na madereva wote kuzingatia masharti ya leseni zao kwani tutaendelea kuwachukulia hatua kali”. alisema RTO Bukombe.

Aidha ameendelea kutoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya usafiri hasa mabasi kuwasimamia madereva na Makondakta ili kuepukana na usumbufu wa mara kwa mara utakaojitokeza.

Ameongeza kuwa endapo watawasimamia vizuri  watafuata sheria zote za barabarani zilizowekwa . Pia amewataka kuyafanyia matengenezo ya mara kwa mara.

Madereva na Makondakta wa mabasi hayo walikamatwa kwa ajili ya mahojiano na kisha walipewa dhamana ili waweze kuwafikisha abiria sehemu wanazoelekea na baadaye wametakiwa kurudi kituo cha Polisi kwa hatua zaidi za kisheria. Aidha abiria waliozidi katika mabasi hayo walirudishiwa nauli zao.


from sokoa news https://ift.tt/2O46CzS
1

Post a Comment

0 Comments