KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema amefanya kazi kubwa kumrejesha Haruna Niyonzima, katika kiwango chake, akimmwagia sifa kama mmoja wa wachezaji bora kuwahi kukutana nao.
Niyonzima alipotezewa na kocha wa zamani wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, ambaye alikuwa akimshutumu kiungo huyo kuwa hana nidhamu.
Akizungumza nasi juzi alipoulizwa iwapo kiungo huyo ana nafasi katika kikosi chake msimu ujao, Aussems aling’aka: “Niyonzima? Hawezi kwenda kokote, ataendelea kuwapo Simba kwani ni mchezaji mzuri na muhimu katika kikosi changu.”
Kocha huyo alisema kutokana na uzoefu wake wa kusoma tabia za wachezaji pamoja na uwezo wao, aligundua Niyonzima ni bonge la mchezaji na kuamua kumfungia kazi.
“Mara nyingi alikuwa akija mazoezini alionekana kama amekata tamaa, lakini siku moja nilipata muda wa kukaa naye na akanieleza kila kitu kuhusu yeye, ilifikia wakati alitaka kuachana na mpira arudi kwao (Rwanda).
“Lakini nilimweleza kwamba muda wake bado asahau yaliyopita, tuanze upya na kwamba angerejea katika kiwango chake, nashukuru kwa sasa namwona vile ambavyo anapambana, nina imani ameiva na hatarudi nyuma tena,” alisema huyo.
Aidha, Aussems, alisema Niyonzima ana kipaji cha aina yake, lakini kwa mwalimu asiye na uelewa wa haraka, ni rahisi kumpoteza.
Kwa upande wa tabia ya Niyonzima, Aussems, alisema kuwa ni mchezaji mwenye busara na kutekeleza kwa haraka maagizo anayopewa na kiongozi wake.
“Nakaribia kumaliza msimu sasa tangu nimeanza kuifundisha Simba, sijawahi kumwona akipinga jambo lenye msingi, leo hii hata nikiondoka Simba, najua hawezi kutetereka tena,” alisema Aussems.
Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Niyonzima alicheza vizuri mno na kuchangia kwa kiasi kikubwa ushindi walioupata wa mabao 2-1 uliowawezesha kutinga robo fainali.
Akizungumzia kiwango chake hicho, Niyonzima, amesema kuwa iwapo Aussems ataendelea kumpa nafasi, Wanamsimbazi watarajie makubwa zaidi kutoka kwake.
“Kinachokatisha tamaa ni kuona una uwezo wa kuisaidia timu yako, lakini nafasi ya kucheza unakosa, likitokea jambo hili mara mbili, tatu, ni wazi kiwango chako kitashuka,” alisema Niyonzima aliyewahi kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa.
0 Comments