Habari Mpya Kutoka Yanga Iliyotufikia Hivi punde Toka Mwanza




KIKOSI cha Yanga kimetua jijini hapa jana na kupata mapokezi ya aina yake, huku wazee wa klabu hiyo wa Mwanza wakiwahakikishia mashabiki wao kufanya kila linalowezekana ili kila mechi watakayocheza Uwanja wa CCM Kirumba, wanashinda.

Kesho Yanga itacheza na wenyeji Alliance katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam kwenye uwanja huo.


Ikumbukwe kuwa Yanga watakuwa wakiutumia CCM Kirumba kama uwanja wao wa nyumbani kupisha maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, itakayochezwa kwenye uwanja ule wa Taifa, Dar es Salaam unaotumiwa na Wanajangwani hao.

Msafara wa Yanga ulitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza saa 1:30 asubuhi, huku ukimkosa nahodha wa kikosi hicho, Ibrahim Ajib, ambaye mara kadhaa amehusishwa na tetesi za kurejea Simba.

Walipoingia katikati ya jiji, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, watoto, vijana na wazee, walijipanga mistari miwili na kuacha nafasi ya wachezaji kupita (guard of honor), kisha kuelekea katika Hoteli ya JB Belmont iliyoko Barabara ya Kenyatta kwa ajili ya mapumziko na jioni walitarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Nyamagana.

Akizungumzia kukosekana kwa Ajib, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema wamemwacha Dar es Salaam nyota wao huyo kwa kuwa hayupo fiti baada ya kuwa nje ya uwanja kwa siku kadhaa kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimkabili.

“Hatujaambatana na Ajib kwa sababu alianza mazoezi juzi (Jumanne), hakuwa vizuri, hawezi kuja kwa sababu hajafanya mazoezi ya kutosha, lakini wachezaji wengine waliokuwa na timu ya taifa, tuko nao,” alisema.

Akizungumzia mchezo wao wa kesho, Zahera, alisemaanatambua Alliance waliokuwa kambini nchini Rwanda si wa kubeza, akisisitiza wamekuja Mwanza ili kuipeleka timu yake hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

“Kwa leo (jana) tutakuwa na mazoezi ya kawaida tu ya mbinu za mchezo, kuangalia namna ambavyo Alliance wanacheza, lakini kesho (leo) tunafanya mazoezi ya kunyoosha viungo tu na kuutuliza mwili, halafu tunapumzika kwa ajili ya mechi,” alisema.

Katika kuonyesha jinsi walivyofurahia ujio wa Yanga jijini hapa, hasa uamuzi wa kutumia CCM Kirumba kama uwanja wao wa nyumbani, mashabiki wa klabu hiyo wa Mwanza na maeneo ya jirani, wameahidi kutowaangusha wenzao.

“Tumefurahi timu yetu kuja kuweka kambi hapa Mwanza, tutaungana wazee wote wa Mwanza kwa kushirikiana na vijana kuona ni kwa namna gani tunaisapoti Yanga yetu iweze kushinda kila mechi, tukianzia na hii ya Jumamosi (dhidi ya Alliance),” alisema mmoja wa wanachama wa Yanga aliyejitambulisha kwa jina na Mzee George Shija.

Mwanachama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Rashid Chuma wa Nyakato, alisema: “Wanachama na mashabiki wa Mwanza tunatakiwa kuungana kuiwezesha Yanga kushinda mechi zote zitakazochezwa CCM Kirumba, itakuwa ni aibu kama timu itapoteza mechi ikiwa mikononi mwetu.

“Wenzetu wa Dar es Salaam na mikoa mingine wamefanya kazi kubwa, hivyo sasa ni zamu yetu kuonyesha mapenzi yetu kwa timu yetu ya Yanga.”a
1

Post a Comment

0 Comments