Simba yageuka Mtaji DRC Congo



SIMBA imeendelea kuwa mtaji kwa mashabiki wa soka DR Congo ambapo mwishoni mwa wiki hii, wanatarajia kupata uhondo wa aina yake kutoka kwa TP Mazembe ambao wamekiri kupania kuonyesha kandanda la hali ya juu dhidi ya FC Lupopo kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao wa wiki ijayo dhidi ya Wekundu wa Msimbazi hao.

Mchezo baina ya Simba na TP Mazembe utakaopigwa Aprili 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ni wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku timu zote hizo zikiwa zimepania kushinda ili kutinga nusu fainali.


Kwa kufahamu moto wa Simba waliouonyesha tangu mwanzoni mwa michuano hiyo ya Afrika, TP Mazembe wameweka wazi kuwa mchezo wao wa kesho dhidi ya wapinzani wao hao katika Ligi ya DR Congo, ni fursa pekee ya kufahamu ni vipi watakabiliana na Simba.

Akizungumza mjini Lubumbashi jana, Kocha wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo Kazembe, aliyezaliwaSeptemba 17, 1976 mjini Lubumbashi, alisema mechi yao ya kesho itakuwa ni tofauti kabisa na zilizopita hivyo mashabiki wao watarajie burudani ya aina yake.

Kazembe aliyewahi kuwa kiungo wa timu hiyo iliyoichezea mechi za Klabu Bingwa ya Dunia mara mbili, mwaka 2010 alipokuwa nahodha, wanatakiwa kutumia mbinu na ufundi wao wote kesho kuona kama unaweza kuwasaidia watakapovaana na Simba.

“Tunapojiandaa kusafiri hadi Dar es Salaam kuifuata Simba, tunatakiwa tuwe katika hali nzuri tuweze kushinda. Iwapo tutafanya kosa lolote na kupoteza pointi (kesho), hii inaweza kutuathiri katika mipango yetu ya kufikia malengo yetu,” alisema Kazembe aliyewahi kufanya majaribio Arsenal ya England.

Aliongeza: “Ni heshima kubwa kwetu kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mwaka jana tulishindwa kuvuka robo fainali, huwezi kukubali hilo litokee tena. Ndio maana tumejipanga kuonyesha ubora wetu Jumamosi (kesho) kwani ushindi utawawezesha wachezaji wetu kwenda Tanzania wakiwa na morali ya hali ya juu.”

Kazembe alisema baada ya kuwakosa baadhi ya nyota wao wa kigeni katika mchezo wao wa ligi wa Jumatano iliyopita, wanatarajia kuwa nao kesho na hata watakapoifuata Simba.

Aliwataja wakali wao hao kuwa ni Treasure Mputu, Meschak Elia, Djos Issama, Kabaso Chongo na Joseph Ochaya, ambao tayari wamewasili Lubumbashi na kuanza mazoezi na wenzao.

Pia, wachezaji wao wanaounda kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 23 cha DR Congo, Arsene Zola, Glody Likonza na Jackson Muleka, waliokuwa wamesafiri hadi Morocco kuwavaa wenzao wa huko, walitarajiwa kurejea jana kuungana na kikosi hicho kama ilivyokuwa kwa Sylvain Gbohouo aliyekuwa akiichezea timu yake ya taifa ya Ivory Coast dhidi ya Liberia.

Wakati hayo yakiendelea huko DR Congo, kikosi cha Simba kiliendelea na mazoezi jana kwenye Uwanja wa Boko Veterans, Dar es Salaam tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.

Akizungumza nasi jana, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema vijana wake wapo fiti kwa mchezo dhidi ya Mbao na hata TP Mazembe.

“Tunaendelea vuziri na maandalizi ya mechi zote mbili (dhidi ya Mbao na TP Mazembe), lengo letu ni lile lile kushinda kila mchezo ulio mbele yetu na hatimaye tuweze kutwaa ubingwa wa ligi ya nyumbani na taji la Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Kwa upande wake, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wataambatana na wachezaji wao wote, wakiwamo nyota wa kimataifa waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa.

Alisema kikosi hicho kitaondoka leo asubuhi baada ya mazoezi tayari kuonyeshana kazi na wababe wao hao waliowafunga katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, mwaka jana.
1

Post a Comment

0 Comments