HERITIER Makambo wa Yanga, anaonekana kuwa vizuri katika kufunga mabao msimu huu na kuwazidi ujanja washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na John Bocco.
Licha ya kwamba Makambo raia wa DR Congo na Kagere kuwa sawa kwa mabao, lakini Makambo ni habari nyingine kutokana na takwimu kumbeba.
Wawili hao wakiwa na mabao 14, wanaonekana kukimbizana kwa kasi wote wakitaka kukaa juu ya Salim Aiyee wa Mwadui ambaye kwa sasa anaongoza akiwa na mabao 16.
Takwimu za mabao yao zinaonyesha kuwa, Makambo aliyejiunga na Yanga msimu huu, katika mabao hayo hakuna hata moja alilofunga kwa penalti. Wadau mbalimbali wa soka wanasema kwamba mabao ya penalti ni ya kupewa, hivyo Makambo hajapewa hata bao moja la aina hiyo.
Upande wa Kagere raia wa Rwanda ambaye naye amejiunga na Simba msimu huu, katika mabao yake 14, mawili ameyafunga kwa penalti.
Alianza vizuri kwa kuepuka kufunga kwa penalti kwani mabao 12 yaliyopita aliyafunga kwa njia ya kawaida, lakini yale mawili ya hivi karibuni yaliyomfanya afikishe 14, ameyafunga kwa penalti.
Bocco ambaye ni nahodha wa Simba, anashika nafasi ya nne kwa ufungaji kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa na mabao 11, katika mabao hayo, matatu ameyafunga kwa penalti.
Licha ya wikiendi iliyopita kukosa mkwaju wa penalti kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, lakini Bocco ni fundi wa penalti kutokana na kufunga zote kwenye ligi msimu huu.
Achana na hao wote, wakati Makambo akitamba kwamba mabao yake wala hajasubiri nguvu ya mwamuzi kuzawadiwa, mbabe wao ni Aiyee kwani mabao yake yote 16, hakuna hata moja la penalti.
0 Comments