YANGA kwa sasa wamebakisha mechi nane tu wamalize ligi msimu huu wa 2018/19, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera amechungulia mbali na kuweka bayana kwamba viporo vya Simba vinamtisha kwani wakishinda vyote timu yake haitaambulia kitu.
Kwa sasa Yanga ndiyo wameendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi wakiwa na pointi zao 71 wakiwa wamecheza mechi 30. Wakati Yanga wamecheza mechi hizo Simba wenyewe wanakamata nafasi ya tatu katika ligi wakiwa na pointi 57 baada ya mechi ya mechi 22. Simba wao wamebakisha mechi 16 kabla ya kumaliza ligi.
Kocha huyo raia wa DR Congo amefunguka kuwa anatishwa na hali hiyo kwa sababu mechi hizo 16 ni nyingi kulinganisha na zao nane.
“Hizi mechi 16 ni nyingi sana kwa Simba, ni sawa kabisa na nusu ya michezo ya ligi ambayo timu zinatakiwa zicheze, mimi sikuona sababu hadi sasa timu inakuwa na mechi nyingi namna hii.
“Hali hii inaweza kusababisha matatizo kwetu kama ikitokea kwamba wakashinda mechi zote. Kushinda mechi hizo kwa sasa kwao ni rahisi japo mara ya kwanza tu kwenye mechi 10 mfululizo walishindwa kushinda zote.
“Yaani ni kama ilipangwa watu wengine wacheze wabakishe mechi chache wakati wengine wakiwa na rundo la mechi, mechi zao hizo wakishinda zote ni rahisi tu kwao kuweza kutwaa ubingwa,” alisema Zahera.
0 Comments