YANGA YAKUSANYA MIL 500 KWA SIKU, WACHEZAJI WALIPWA MISHAHARA



KAMATI ya Uhamasishaji ya Yanga iliyo chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera juzi imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 500.

Fedha hizo, zilikusanywa katika uzinduzi wa uhamasishaji huo wa fedha uliofanyika huko mkoani Dodoma chini ya mwenyekiti wake Naibu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde.

Baada ya fedha hizo kukusanywa, hivi sasa Yanga itakuwa imefikisha shilingi milioni 560 ambazo tayari imekusanya baada ya mwezi uliopita kukusanya mil 60, 089, 047 kupitia TigoPesa, M-Pesa na kupitia akaunti ya CRDB ambazo zitatumika kwa ajili ya kusajili wachezaji katika msimu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu na kuthibitishwa na Zahera, fedha hizo zilizopatikana ni sehemu ya ahadi iliyotolewa na wanachama wa Yanga wakiwemo baadhi ya wabunge wa nchini.

Zahera alisema, amefurahishwa na aina ya uendeshaji wa Yanga hivi sasa kupitia wanachama wake wanaosaidia kufanikisha baadhi ya vitu ikiwemo usajili.

“Muda mrefu nilikuwa najiuliza kuna ulazima gani klabu kubwa kama hii ya Yanga isubirie tajiri mmoja aje awekeze fedha zake wakati ina mtaji kubwa wa mashabiki.

“Wao wenyewe wanasema kuwa hii ni timu ya wananchi, kwa nini wananchi tusiibebe timu yetu wenyewe? Sasa tunapaswa kuibeba wenyewe, timu kama Yanga inapaswa kushindania makombe makubwa Afrika, hivyo ninaomba tuichangie Yanga.

“Ninaamini msimu ujao hamtaumia sana, miezi saba niliyokaa hapa tayari nimeshajifunza mazingira na jinsi ligi inavyoendeshwa, hivyo msiwe na hofu, tarajieni mengi kutoka kwangu, ninawashukuru mashabiki wa Yanga wakiwemo wabunge na viongozi wa juu wa serikali kufanikisha hilo la michango,” alisema Zahera.

Baadhi ya viongozi wa juu waliotajwa kuichangia Yanga katika uzinduzi huo wa uhamasishaji wa fedha ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ambaye ameahidi kuichangia na Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali ambao kila mmoja amechangia Sh milioni 10.
1

Post a Comment

0 Comments