Mfungaji bora wa TP Mazembe, Tresor Mputu amesema Simba ni timu tishio katika ukanda wa Afrika.
Akizungumza Dar es Salaam, Mputu alisema wanaifahamu Simba ni timu yenye rekodi nzuri katika mashindano ya kimataifa, hivyo watacheza kwa tahadhari katika mchezo wao wa kesho, Jumamosi
Simba na TP Mazembe ya DR Congo, zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mputu alisema kitendo cha Simba kufika hatua ya robo fainali, kinaonyesha namna ilivyo timu bora inayoundwa na wachezaji wenye viwango bora.
Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao manne katika mashindano hayo msimu huu, alisema Simba ni timu bora hasa inapocheza nyumbani, lakini watapambana kupata matokeo mazuri.
Alisema wamechukua tahadhari baada ya wapinzani wao nchini DR Congo AS Vita kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi jijini Dar es Salaam.
“Tumekuja kushindana hapa ugenini ili kupata matokeo yatakayokuwa na faida kwetu na kuturahisishia katika mchezo wa marudiano nyumbani. Hadi Simba imefikia hatua hii ujue ni timu ya namna gani,” alisema Mputu. Mputu alichangia mafanikio ya TP Mazembe katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumaliza ikiwa na pointi 11 katika Kundi C.
Kiungo huyo alianza kucheza soka ya ushindani katika klabu ya Kin City ya DR Congo mwaka 2000 kabla ya kujiunga na TP Mazembe aliyocheza hadi 2014 akicheza jumla ya mechi 292 akifunga mabao 144.
Mwaka 2014 alijiunga na Kabuscorp ya Angola alikocheza kwa miaka miwili akifunga mabao 18 katika mechi 49 alizocheza. 2016 alirejea TP Mazembe na kuifungia mabao 12 katika mechi 27. Pia amefunga mabao 14 katika 47 za timu ya Taifa ya DR Congo. Mputu amefunga mabao 56 katika muda wote kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema watacheza mechi ngumu na timu bora ambayo inafahamu umuhimu wa mashindano ya kimataifa.
“Kweli tuliifunga AS Vita wanatoka nchi moja na TP Mazembe tutaingia katika mechi zote mbili kwa aina tofauti ya uchezaji ili kupata matokeo ya aina nyingine,” alisema Aussems jana.
Kocha wa zamani wa Yanga Kenny Mwaisabula alisema Simba inatakiwa kutumia kila nafasi ambayo watapata kufunga bao ili kuwa na mtaji mzuri wa mabao na kujiweka katika mazingira mazuri kwa mechi ya marudiano.1
0 Comments