KWA miaka kibao sasa, Ligi Kuu England imekuwa kivutio kwa mastaa wengi wenye vipaji kuja kucheza katika ligi hiyo na kuifanya kuwa na mvuto.
Lakini, sasa kuna uwezekano mkubwa baadhi ya mastaa wa maana wakaachana na ligi hiyo mwishoni mwa msimu huu wakati dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa. Eden Hazard na Paul Pogba ni miongoni tu mwa mastaa wa maana wanaotajwa huenda wakaipa kisogo Ligi Kuu England kwenye dirisha lijalo na kwenda kutoa burudani zao kwenye ligi za nchi nyingine.
Kiungo mtamu wa Arsenal, Aaron Ramsey hatakuwapo tena kwenye Ligi Kuu England msimu ujao na badala yake atakuwa huko kwenye Serie A baada ya kukubali kujiunga na Juventus. Sambamba na hilo, hii hapa orodha ya mastaa wa maana wanaotajwa huenda wakaipiga kibuti Ligi Kuu England kwenye dirisha lijalo na kuondoa mambo yao matamu yaliyokuwa yakiwapa raha mashabiki wa England kila wiki.
Paul Pogba (Man United)
Mashabiki wa Manchester United bila shaka kwa sasa watakuwa wakiishi kwa matumaini juu ya kiungo wao, Paul Pogba baada ya kudai hivi karibuni kuna uwezekano mkubwa wa kwenda kujiunga na Real Madrid. Lakini, kinachotishia zaidi hata kocha wa Real Madrid mwenyewe, Zinedine Zidane ameweka wazi matamanio yake ya kuwa na huduma ya kiungo huyo Mfaransa kwenye kikosi chake huko Bernabeu. Baada ya kurudi kwenye kiwango chake bora tangu kocha Ole Gunnar Solskjaer alipotua Man United, Pogba ameonekanna kama vile atabaki kwa muda mrefu Old Trafford, lakini hilo litategemea zaidi na nafasi ya timu watakayoshika kwenye msimamo. Kama hakutakuwa na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao basi kuna uwezekano mkubwa, Pogba akashawishika na uamuzi wa kuondoka kwenye timu hiyo na kutimkia Bernabeu.
Wilfried Zaha (Crystal Palace)
Kufanikiwa kwa wachezaji wa Kingereza huko Ujerumani kumedaiwa kuchochea mashabiki wa soka wa nchi hiyo kuanza kuzifuatilia timu za huko. Baada ya Jadon Sancho kufanya kweli huko Borussia Dortmund na Reece Oxford akitamba na Borussia Monchengladbach, huku staa aliyetolewa kwa mkopo na Arsenal, Reiss Nelson akitesa Hoffenheim kumefungua njia ya Waingereza wengi kuanza kuifuatilia Bundesliga. Kutokana na hilo, staa mwingine wa kutoka kwenye Ligi Kuu England, Wilfried Zaha amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Borussia Dortmund. Kinachoelezwa ni kwamba Zaha anaweza kwenda zake kutimkia Signal Iduna Park, licha ya kwamba jambo hilo halina uhakika kwa asilimia mia, huku Manchester United wakitajwa pia kuwa mpango wa kunasa huduma ya mchezaji huyo anayetamba huko Selhurst Park.
Idrissa Gana Gueye (Everton)
Suala la Paris Saint-Germain kusajili wachezaji inaowataka kimekuwa kitu chepesi kwa miaka ya karibuni kwa sababu wachezaji kibao wanapenda kwenda kujiunga na timu hiyo. Baada ya kufanikiwa kuwanasa Neymar na Kylian Mbappe, suala la PSG kumsajili mchezaji wanayemtaka limekuwa jepesi huku ikielezwa kwamba kocha Thomas Tuchel anahitaji kufanya maboresho makubwa kwenye sehemu ya kiungo ya timu yake. Katika mpango huo, kiungo wa zamani wa Aston Villa, Gueye yupo kwenye rada na baada ya kuwashindwa kuwashawishi Everton kwenye dirisha la Januari, bila shaka jambo lake litamalizwa katika usajili ujao. Kocha Marco Silva aligoma kumpoteza mchezaji wake muhimu kama Gueye kwenye dirisha la katikati ya msimu, lakini mwisho wa msimu basi huenda uhamisho wa mchezaji huyo kuachana na maisha ya Goodison Park yakatimia.
Sadio Mane (Liverpool)
Baada ya Mohamed Salah kuonekana kushuka kidogo kiwango chake cha kufunga, mshambuliaji Sadio Mane sasa amekuwa mtu wa kuibeba Liverpool kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Rekodi zake kwenye mechi kubwa zimekuwa na mvuto kweli kweli na hilo alilionyesha vyema kabisa kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich na kuifanya Liverpool kusonga mbele. Na kama inavyoelezwa kwamba kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amepanga kuijenga upya timu hiyo na huenda mmoja wa wachezaji wanaotajwa kwamba watabebwa wakacheze huko Bernabeu atakuwa Msenegali huyo. Kinachoelezwa ni kwamba Mane alikuwa kwenye mipango ya Real Madrid tangu alipokuwa kwenye kikosi cha Southampton na mambo yanaweza kukamilishwa kwenye dirisha lijalo la usajili, Mane akitimkia zake Bernabeu.
Marko Arnautovic (West Ham)
Kama shabiki wa soka anataka kufahamu namna gani matukio ya mchezo huo yanavyoweza kubadilika kwa haraka sana basi mshambuliaji Marko Arnautovic ni mfano mzuri. Katika majira ya kiangazi ya mwaka 2017, fowadi huyo alikwenda kujiunga na West Ham United akitokea Stoke City kwa ada iliyoweka rekodi kwenye klabu hiyo. Miezi 12 baadaye, mshambuliaji huyo alilazimisha dili la kwenda China na kugomea baadhi ya mambo kwenye kikosi hicho. Lakini, baada ya dili kukwama, staa huyo aliwaomba radhi mashabiki wa timu na kubaki. Hata hivyo, kinachoelezwa ni kwamba staa huyo hana muda mrefu wa kuendelea kubaki kwenye timu hiyo na huenda mwishoni mwa msimu huu atatimiza ndoto zake za kuondoka West Ham na kutimkia China kwenye dili za pesa ndefu.
Abdoulaye Doucoure (Watford)
Tangu alipoanza kuichezea Watford miaka mitatu iliyopita, kiungo Doucoure amekuwa akihusishwa na mpango wa kuihama timu hiyo. Kiungo huyo alijiunga na Watford mwaka 2016, kisha akatolewa kwa mkopo Granada. Akicheza soka la kutumia nguvu na ufundi, huku mwenye macho ya kulioga goli, kumeibuka maneno kwamba vigogo wa Ligi Kuu England, Liverpool na Manchester United zinahitaji saini huduma ya kiungo hasa baada ya kufurahishwa na kiwango chake cha ndani ya uwanja. Lakini, pia kiungo huyo yupo kwenye rada za klabu za ng’ambo kama vile PSG, ambao kwenye dirisha lijalo la usajili wataingia sokoni kusaka staa wa kwenda kuziba pengo la Adrien Rabiot, anayeondoka baada ya msimu huu kumalizika.
Ander Herrera (Man United)
Kwa namna Ander Herrera alivyopambana kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Manchester United na kukamatia sehemu ya kiungo ni kitu kinachovutia sana. Amepambana kiume na sasa mashabiki na hata kocha wao hakuna kitu asichopenda kusikia masikioni mwake kama habari za kwamba ataondoka. Kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa sasa anachokiamini kuhusu Mhispaniola huyo ni kwamba anastahili nafasi ya kuendelea kubaki kwa muda mrefu huko Old Trafford. Lakini, sasa mkataba wake utafika tamati mwisho wa msimu huu na hakuna dili jipya lilizongumzwa na kuafikiana jambo linalozifanya klabu nyingine vigogo kama vile PSG kuhitaji saini yake. Kinachoonekana ni wazi kabisa, Herrera anaweza kuachana na Man United, kuna asilimia kubwa ya jambo hilo.
Eden Hazard (Chelsea)
Kama mashabiki wa Manchester United wanaumizwa na hizo habari za kwamba kiungo wao Paul Pogba anaweza kwenda Real Madrid basi hao wa Chelsea watakuwa kwenye hali gani? Hazard amekuwa na mapenzi ya Real Madrid kwa miaka mingi sana na hakutaka kuweka kificho kwamba anamkubali kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane.
Wakati kocha Maurizio Sarri akielekea mlango ulioandikwa ‘exit’, staa wa Kibelgiji, naye jicho yale moja tayari limeshaanza kuutazama mlango huo wa kutokea huko Stamford Bridge. Kitu pekee kinachoweza kumzuia Hazard asiondoke ni adhabu ya Chelsea kufungiwa kusajili aamue kuwa muungwana tu kama alivyofanya Antoine Griezmann huko Atletico Madrid.1
0 Comments