
BEKI wa Simba, Pascal Wawa, amesema kwa kuwa klabu yake hiyo bado imekaa kimya juu yake, anaendelea kukaribisha ofa zaidi kutoka kwingikeo, wakiwamo Yanga ambao msimu uliopita walimtaka bila mafanikio.
Hata hivyo, pamoja na mchezaji huyo kupokea ofa lukuki, amekiri kuwapa nafasi ya kwanza Wekundu wa Msimbazi.
Wawa alisajiliwa na Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja, akiwa mchezaji huru baada ya kukaa msimu mzima bila ya kucheza.
Akizungumza na BINGWA jana, Wawa alisema bado hajafanya mazungumzo na Simba, hivyo anaendelea kuwasikilizia kwa sababu muda bado upo.
“Kuna klabu ambazo zinanihitaji, lakini nafasi ya kwanza bado naipa Simba, hivyo siwezi kusaini kwanza sehemu nyingine kwa sababu bado napenda kucheza kwenye timu yangu,” alisema na kuongeza:
“Kama Simba wataendelea kuwa kimya, itabidi nikaribishe klabu nyingine zije mezani tuongee maana mpira ndio kazi yangu.”
Alipotakiwa kutaja klabu zinazomwania, alisema hawezi kuweka wazi hilo hadi atakapofahamu mwafaka wake ndani ya Simba.
Beki huyo kisiki raia wa Ivory Coast, ameisaidia mno Simba kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, huku akiiwezesha timu hiyo kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
from sokoa news http://bit.ly/2ZgFu0X
1

0 Comments