Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama ameliagiza Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi (NEEC), kuwaondoa waratibu wa uwezeshaji wa mikoa, ambao wanashindwa kuwajibika.
Pia amewaonya vijana wanaoshiriki mafunzo ya ujasiriamali, watakaoshindwa kupiga hatua na kupuuza mafunzo wanayopewa huku akisisitiza kuwa atawashughulikia.
Mhagama alitoa agizo hilo jana jijini hapa, alipokuwa akizindua mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana, kutokana na baadhi ya mikoa kutokuwa na wawakilishi katika mafunzo hayo.
Alisema baadhi ya waratibu wa madawati ya uwezeshaji wananchi, wamekuwa hawawajibiki ipasavyo katika kuwasaidia wananchi, ikiwamo wale ambao mikoa yao imeshindwa kuwakilishwa katika mafunzo hayo, ambayo yanajumuisha vijana kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara.
"Kuna baadhi ya mikoa nimeiandika hapa imeshindwa kuleta vijana kwenye mafunzo haya, hivyo waratibu wa mikoa hiyo ambao watabainika wameshindwa kuleta wawakilishi kwa uzembe waondolewe kwenye nafasi zao, sambamba na wale wanaoshindwa kuwajibika kwa wananchi," alisema.
Baadhi ya mikoa ambayo ilishindwa kuwa na wawakilishi kwenye mafunzo hayo ni Dar es Salaam, Rukwa, Pwani, Singida, Iringa na Njombe.
Aidha, Jenista pia ameliagiza Baraza hilo, linawaunganisha vijana wote waliopata mafunzo na taasisi za fedha na kuhimiza haja ya taasisi hizo kuja na riba na masharti rafiki kwa vijana. Aliwataka vijana ambao watapata fursa za mikopo, kujenga nidhamu ya kurudisha mikopo.
from sokoa news https://ift.tt/2KbDDVB
1
0 Comments